Jumatatu , 15th Oct , 2018

Imeelezwa kuwa Tanzania iko salama kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki hakuna matukio ya kigaidi tofauti na nchi nyingine za ukanda huo ikiwemo Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.

Akizungumza kupitia East Africa BreakFast, Inspekta Damasi Cosmas Nyangula mmoja kati ya askari kutoka kikosi cha polisi wasio na mipaka 'Interpol' amesema kuwa licha ya kuibuka kwa matukio ya kiuhalifu hivi karibuni lakini bado nchi iko salama na haina matukio ya kutisha kama nchi za jirani.

"Kupitia kikosi cha polisi wasio na mipaka nchi imenufaika na vitu vingi, ikiwemo askari wake kupewa mafunzo ya kukabiliana na uhalifu, ukizingatia dunia sasa inakabiliwa na matukio ya kigaidi", amesema Inspekta Nyangula.

Akizungumzia kuhusu ni mavazi gani ambayo yanawatambulisha askari wa kikosi hicho amesema kuwa, "'Interpol' au askari wasio na mipaka ni kikosi ambacho kiko chini ya mkurugenzi wa makosa na upelelezi, kazi yetu kubwa ni kuratibu na kupeleleza makosa ya kijinai na hatuvai sare kwakuwa tunakabiliwa na vitisho".

Inspekta Nyangula amesema kuwa  kikosi hicho kinafanyakazi endapo mtuhumiwa ametoka nje ya nchi na kukimbilia nchini au nje lakini kwa makosa ya ndani hawashughuliki kwani kuna jeshi la polisi linafanya kazi na watuhumiwa wa ndani.

"Tunafanya kazi duniani kote kwa kutumia namna mbili za ushirikiano, moja ni wa kipolisi na mwingine ni wa kutumia ofisi ya mwanasheria mkuu wa nchi husika hivyo kupatiwa ushirikiano wote katika utekelezaji wa majukumu yetu bila mipaka", amesema Inspekta Nyangula.

'Interpol' au askari wasio na mipaka ni kikosi ambacho kiko chini ya mkurugenzi wa makosa na upelelezi, kazi yao  kubwa ni kuratibu na kupeleleza makosa ya kijinai ikiwemo matukio ya kigaidi katika nchi wananchama wa jumuiya hiyo duniani.